HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA, MHE. CHARLES N. KEENJA (MB.) WAKATI AKIWASILISHA MUSWADA WA SHERIA YA HAKI
MILIKI ZA WAZALISHAJI WA AINA MPYA ZA MBEGU NA MIMEA (PROTECTION OF NEW PLANT
VARIETIES (PLANT BREEDERS RIGHTS) ACT, 2002) MBELE YA KAMATI YA BUNGE YA
UCHUMI NA FEDHA
__________________________________________
1.0
Utangulizi
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada wa sheria ya Haki Miliki za Wazalishaji wa Aina
Mpya za Mbegu na Mimea (Protection of New Plant Varieties (Plant
Breeders Rights) Act, 2002) unakusudia kutunga sheria itakayoweka
utaratibu wa kusajili haki miliki za
wazalishaji wa mbegu na mimea mipya, ili kuharakisha na kuboresha
maendeleo ya kilimo kupitia kwa watafiti, wazalishaji na waendelezaji wa mbegu
na mimea mipya. Utaratibu huo utahakikisha kuwa watafiti, wazalishaji na
waendelezaji wa mbegu na mimea mipya
wanakuwa na haki ya kunufaika na kazi walizozifanya za utafiti,
uzalishaji na uendelezaji wa mbegu na mimea mipya, kabla ya mtu mwingine yeyote. Aidha, Muswada unakusudia kuanzisha ofisi ya
Msajili wa haki miliki itakayohusika na usajili na
usimamizi wa haki miliki za mbegu na mimea mipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya kuweka
utaratibu wa utoaji wa haki miliki za
wazalishaji na watafiti wa mbegu na
mimea mipya ni muhimu baada ya Serikali kuruhusu sekta binafsi kujihusisha na
biashara ya mbegu, kuanzia mwaka wa 1993. Mfumo wa
awali uliipa Serikali haki pekee ya kumiliki utafiti, uzalishaji, uuzaji,
ununuzi na usambazaji wa mbegu. Mfumo huo ulisababisha mbegu zote
zilizozalishwa, ikiwa ni pamoja na mbegu mpya,
kutotosheleza mahitaji ya wakulima. Aidha, watafiti na
wazalishaji wa mbegu na mimea mipya hawakunufaika moja kwa moja kwa kuwa
walikuwa hawapati mapato yoyote kutokana na ugunduzi wao. Shughuli za
uzalishaji na uendelezaji wa mbegu na mimea mipya
zilikuwa zikifanywa na vituo vya utafiti na mashamba ya Serikali na hatimaye
kusambazwa na Kampuni ya mbegu ya Taifa (TANSEED). Baada ya kuanzisha mfumo wa kuzalisha mbegu
na mimea mipya na kuzisambaza kwa kuhusisha sekta binafsi, kumekuwa hakuna
sheria yenye kukidhi mahitaji ya kulinda haki za wazalishaji wa mbegu za
Serikali na za wazalishaji wa mbegu binafsi, pamoja na kudhibiti usambazaji wa
mbegu na mimea mipya. Matokeo yake wazalishaji wa
mbegu binafsi wamekuwa wakisita kuwekeza ipasavyo kwenye utafiti wa mbegu.
Aidha, kuna hatari ya mbegu mpya zinazozalishwa na Serikali kuibiwa kabla
Serikali haijafaidika
nazo ipasavyo.
2.0
Madhumuni ya Muswada
Mheshmiwa Mwenyekiti, Madhumuni
ya Muswada huu ni kutunga sheria mpya itakayoitwa “Protection of New
Plant Varieties (Plant Breeders Rights) Act, 2002”, itakayotambua haki miliki za wazalishaji wa
mbegu na mimea mipya na itakayokidhi mabadiliko ya kijamii na kiuchumi
kulingana na soko huria la uzalishaji na usambazaji wa mbegu nchini. Haki hizo zitawawezesha wazalishaji wa mimea na mbegu mpya kunufaika na utafiti wao kutokana na
malipo watakayopata kwa kutoa leseni au kuruhusu mbegu zao zitumiwe na
wazalishaji wengine kwa ajili ya biashara (“seed multiplication”).
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Mbegu zilizozalishwa na taasisi za Serikali za utafiti
zitalindwa chini ya Sheria hii na kuiwezesha Serikali kupata mapato kutoka kwa
wazalishaji wa kibiashara watakaoomba na kupewa leseni za kuzalisha au kuuza
mbegu na mimea mipya iliyogunduliwa na watafiti wa Serikali. Aidha, kwa kutumia njia ya kuwasajili wazalishaji wa mbegu na mimea
mipya Serikali itaweza kudhibiti ubora wa mbegu mpya, ikiwa ni pamoja na
kuwadhibiti wazalishaji holela.
3.0
Muundo wa Muswada
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu
umegawanyika katika sehemu kuu kumi na mbili: -
Sehemu ya kwanza inaeleza mambo ya
kiutangulizi yaani:-
·
Jina fupi la sheria na tarehe
ya kuanza kutumika kwa sheria;
·
Tafsiri ya baadhi ya maneno
yaliyotumiwa katika Muswada pia imetolewa.
4.0
Sehemu ya Pili
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya pili inaanzisha ofisi ya
Msajili wa haki miliki za watafiti na waendelezaji wa
mbegu na mimea mipya. Aidha, sehemu hii inabainisha kazi za Msajili na utaratibu wa kusajili mbegu na mimea hiyo. Sehemu hii
vilevile inaanzisha Kamati ya Ushauri wa utoaji wa
haki miliki. Kamati hii itaundwa na wawakilishi kutoka
taasisi zifuatazo:
(i)
Chama
cha wazalishaji wa mbegu na mimea mipya;
(ii)
Chama
cha wakulima wa mbegu;
(iii)
Chama
cha wafanyabiashara wa mbegu;
(iv)
Mwakilishi
wa wakulima;
(v)
Chuo
Kikuu au taasisi inayohusika na utafiti wa kuzalisha mbegu na mimea mipya;
(vi)
Wakala wa utoaji wa haki miliki za gunduzi mbalimbali (intellectual
property rights); na,
(vii)
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za Kamati hii zitakuwa ni pamoja na zifuatazo:
§
Kumshauri
Waziri kuhusu utekelezaji wa sheria;
§
Kupokea
kutoka kwa Msajili na kutoa maoni ya kitaalam kuhusu uhakiki wa hati za maombi
ya haki miliki, kabla hazijasajiliwa;
§
Kumshauri
Msajili kuhusu utoaji wa haki miliki.
5.0
Sehemu ya Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya tatu
inaainisha sifa za mbegu za mazao ambazo zinastahili kusajiliwa na kupata hifadhi ya kisheria. Sehemu hii vilevile ina vipengele vinavyohusu usajili kwa madhumuni maalum.
6.0
Sehemu ya Nne
Mheshimiwa
Mwenyekiti, Sehemu ya nne ina
vipengele vinavyoelezea utaratibu wa kuomba usajili wa haki miliki. Vipengele
hivi ni pamoja na:-
a)
Vipengele vinavyoainisha mambo
yanayopaswa yaonekane kwenye hati za maombi; na
b)
Vipengele vinavyohusu
mapendekezo ya jina la haki miliki inayoombwa.
7.0
Sehemu ya Tano
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya tano
inahusu utaratibu utakaofuatwa na wazalishaji na
waendelezaji wa mbegu na mimea mipya katika kuomba usajili.
Sehemu hii inaainisha mabadiliko katika hati za
maombi anayoweza kufanya muombaji. Pia Sehemu hii ina vipengele
vinavyoonyesha utaratibu utakaotumika katika kutoa haki miliki, ikiwa ni pamoja
na utaratibu na vigezo vitakavyotumika kupinga usajili wa muombaji na namna ya
kutolea uamuzi pingamizi
8.0
Sehemu ya Sita
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu hii ina vipengele kuhusu kuendelea kwa majukumu ya kisheria
yaliyotolewa chini ya Sheria ya Mbegu ya mwaka wa 1973 kuhusu biashara ya mbegu
hapa nchini. Aidha, sehemu hii inaainisha mambo yafuatayo:
a) haki za msingi wanazostahili kupewa
waombaji;
b) muda wa kunufaika na haki hizi, ambao
utakuwa miaka ishirini; na,
c) ada ya
lazima itakayowawezesha wenye haki miliki kuendelea kunufaika na haki miliki
walizopewa.
9.0
Sehemu ya
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya saba inatoa madaraka kwa Msajili kubatilisha haki miliki
10. Sehemu ya Nane
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya nane inatoa
madaraka kwa wenye haki miliki kutoa leseni za uendelezaji wa mbegu au mimea mipya kwa
waendelezaji wa kibiashara. Aidha, sehemu hii inampa uwezo Msajili kumlazimisha
mwenye haki miliki kutoa leseni hiyo
11. Sehemu ya
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya tisa inahusu utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya mtu
yeyote atakayeona kuwa uamuzi uliofanywa chini ya sheria hii sio wa haki.
Sehemu hii pia inampa madaraka Waziri kuteua wajumbe wa
Bodi ya Rufaa Bodi hiyo imeanzishwa chini ya sehemu hii ili kusikiliza na kutoa
uamuzi juu ya malamiko mbalimbali, bila kuathiri haki ya mhusika kukata rufaa
mahakamani juu ya uamuzi utakaotolewa na Bodi.
12. Sehemu ya Kumi
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya kumi inaanzisha
Mfuko utakaotumika katika kusimimia maendeleo ya utoaji haki miliki. Matumizi ya Mfuko yatakuwa ni pamoja na:
(a)
kulipia gharama za kuanzisha na kuendeleza benki ya mimea na
mbegu mpya zitakazosajiliwa chini ya sheria hii;
(b)
kulipia gharama za kuendesha ofisi ya Msajili na kulipia
utoaji wa taarifa kwa watafiti kuhusu haki miliki zilizosajiliwa au
zinazotarajiwa kusajiliwa;
(c)
kusaidia katika kusimamia utekelezaji wa sheria kwa ujumla.
Mapato ya Mfuko huu yatatokana na;
§
ada zitakazokusanywa chini ya sheria hii; na,
§
mikopo au misaada itakayotolewa na watu au taasisi
mbalimbali.
13. Sehemu ya kumi na moja
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya kumi na moja ina
vifungu vinavyoainisha makosa
na adhabu kwa makosa hayo.
14. Sehemu ya Kumi na Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sehemu ya kumi na mbili inahusu vipengele mbalimbali vinavyohitajika katika
kutekeleza sheria hii. Vipengele hivi ni pamoja na
vifuatavyo:
(a) kipengele kinachotoa madaraka kwa Msajili kutathmini na
kukusanya ada kutoka kwa waombaji;
(b) kipengele kinachowataka wahusika katika utekelezaji wa
sheria kutunza siri za maelezo na nyaraka wanazozipata au watakazozitoa;
(c) kipengele kinachompa mamlaka Msajili kusajili haki miliki za
mimea na mbegu mpya zilizozalishwa kabla ya kuanza kwa sheria hii, zikiwemo
mbegu na mimea inayomilikiwa na Serikali;
(d) kipengele kinachompa uwezo Waziri kuweka utaratibu wa
kuhakikisha kuwa wakulima wananufaika na uendelezaji wa mimea na mbegu zitakayosajiliwa
chini ya sheria hii;
(e) kipengele kinachompa uwezo Waziri kutengeneza Kanuni za
kusimamia utekelezaji wa sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba
kuwasilisha.
WAZIRI WA KILIMO NA
CHAKULA
OCTOBA, 2002