HOTUBA YA WAZIRI WA KILIMO NA
CHAKULA, MHE. CHARLES N. KEENJA (MB.), AKIZINDUA BODI YA WAKURUGENZI YA BODI YA
KAHAWA, MOSHI, TAREHE 18 AGOSTI, 2003.
Ndugu
Mwenyekiti, Dr. Hussein Mongi,
Ndugu Wajumbe
wa Bodi
Awali
ya yote, ninapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa kunialika kuja kuzindua
Bodi yenu. Ninapenda kuchukua nafasi hii
kukupongeza wewe Dr. Hussein Mongi kwa kuteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa
Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Kahawa.
Aidha, ninawapongeza Wakurugenzi wote wa Bodi kwa kuteuliwa kuwa wajumbe
wa Bodi ya Wakurugenzi.
2. Ndugu
Mwenyekiti, Bodi ya Kahawa ni chombo muhimu ambacho Serikali imekasimu madaraka
kwake ili kisimamie maendeleo ya zao la kahawa.
Jukumu kubwa la Bodi ni kufanya shughuli zote za lazima na za manufaa
kwa zao la kahawa. Majukumu hayo
yanajumuisha;
(i)
Kuishauri Serikali kuhusu sera na mikakati ya kuendeleza zao
la kahawa ili kuongeza ubora, uzalishaji na ushindani kwenye masoko ya ndani na
nje ya nchi;
(ii)
Kuhimiza uendelezaji wa uzalishaji, usindikaji na soko la kahawa.
(iii)
Kuandaa kanuni za kusimamia taratibu za upandaji na biashara
ya kahawa ikiwa ni pamoja na kufuatilia bei ya zao
(iv)
Kutoa fedha kwa ajili ya utafiti na Maendeleo ya Kahawa
kuhamasisha uuzaji wa kahawa ndani na nje ya nchi.
(v)
Kuweka kanuni na kudhibiti ubora wa kahawa na mazao ya
kahawa.
(vi)
Kukusanya, kuchambua, kutunza, kutumia au kusambaza taarifa
na takwimu zinazohusiana na zao la kahawa.
(vii)
Kufuatilia uzalishaji na uuzaji nje wa kahawa.
(viii)
Kuhimiza uendelezaji wa teknolojia katika sekta ya pamba.
(ix)
Kuandaa kanuni kwa ajili ya usindikaji, uuzaji nje na hifadhi
ya kahawa na mazao yake.
(x)
Kusaidia katika uanzishwaji wa vyama au vyombo vingine
vinavyohusiana au kujihusisha na zao la kahawa.
(xi)
Kulinda maslahi ya wakulima dhidi ya umoja wa wanunuzi ambao
unaweza kufanywa kupitia katika uundwaji wa vyama.
(xii)
Kuhakikisha uendeshaji sahihi wa Mfuko wowote ulioanzishwa
chini ya sheria ya kahawa.
Chombo hiki kina wajibu mkubwa wa
kusimamia shughuli zote za lazima na za manufaa kwa zao la kahawa. Majukumu ya Bodi ya Kahawa yameainishwa
vizuri katika sheria Na. 23 ya mwaka wa 2001.
Baadhi ya majukumu hayo ni;
Ninashauri kuwa kila mjumbe wa Bodi
ya Wakurugenzi apatiwe nakala ya sheria hiyo na aisome kwa makini kwa kuwa
inatoa mwongozo wa kufuatwa na Bodi Mpya ya Wakurugenzi katika kuendeleza zao
la kahawa.
3. Ndugu
Mwenyekiti, zao la kahawa linakabiliwa na matatizo mengi ambayo Bodi yako itabidi
iyawekee utaratibu wa kuyatafutia ufumbuzi wa haraka. Baadhi ya matatizo hayo ni;
(i)
Tija ndogo. Uzalishaji kwa eneo
ni wastani wa kilo 170 kwa hekta, wakati tija inayowezekana ni kilo 600 kwa
hekta. Tija hii ndogo inatokana na
kutofuata kikamilifu kanuni za kilimo bora cha kahawa. Katika baadhi ya maeneo nchini mibuni
imezeeka
(ii)
Matumizi madogo ya pembejeo za kilimo. Kutokana na gharama kubwa za pembejeo,
hususan mbolea na madawa, wakulima wengi wamekuwa wakitumia pembejeo kidogo au
kutotumia pembejeo hizo.
(iii)
Bei ndogo ya kahawa.
Bei ya kahawa katika soko la dunia zimekuwa za chini
(iv)
Ubora hafifu wa kahawa.
Katika miaka ya nyuma, kahawa ya
(v)
Udhaifu katika usimamizi wa soko huru. Kukosekana kwa mfumo wa kusimamia uendelezaji
wa zao la kahawa kuanzia shambani hadi kahawa inapopelekwa mnadani au kwa
ununuzi wa mwisho kumesababisha wafanyabiashara na hata wakulima kuchanganya kahawa ya ubora wa juu na ile ya
ubora wa chini na hivyo kuifanya sehemu kubwa ya kahawa inayozalishwa nchini
kuwa ya ubora wa chini.
(vi)
Huduma duni za ugani.
Kutokana na udhaifu katika kutoa huduma hiyo, mbinu bora za uzalishaji
wa kahawa zimekuwa haziwafikii wakulima.
Aidha, usimamizi mbaya wa kutoa huduma za ugani umechangia sana katika
kudumaza kilimo cha kahawa.
(vii)
Kutokuwapo kwa vinu vya kutosha vya kukoboa kahawa. Katika baadhi ya maeneo wakulima wamekuwa
wakisafirisha kahawa ya maganda umbali mrefu, jambo ambalo linaongeza gharama
za usafirishaji na kumpunguzia kipato mkulima.
(viii)
Mfumo mbaya wa ununuzi wa kahawa.
Wafanyabiashara binafsi wamekuwa wakishirikiana kula njama za kumpa bei
ndogo mkulima. Kutokana na njama hizo,
mnunuzi mmoja hununua kahawa, huikoboa na kwenda kuinunua mwenyewe
mnadani. Njama za namna hiyo zimekuwa zikikwamisha
juhudi za kumpatia mkulima bei nzuri kwa kahawa yake. Kuna taarifa kuwa hata
baada ya kubadilisha utaratibu wa utoaji leseni na kuweka Electronic Auction
Machine kwenye mnada, bado kuna wafanyabiashara wanafanya njama na baadhi
ya wafanyakazi wa Bodi wasiokuwa waaminifu kununua kahawa yao wenyewe kwenye mnada.
(ix)
Magonjwa ya Chulebuni, kutu ya majani na Mnyauko Fuzari wa
Kahawa. Magonjwa hayo yamekuwa
yakiathiri sana uzalishaji wa kahawa nchini.
Kwa mfano, katika Mkoa wa Kagera, kuna ugonjwa wa Mnyauko Fuzari ambao
umesababisha mikahawa mingi kukauka.
(x)
Kodi nyingi kwenye zao la kahawa.
Zao hili limekuwa likitozwa kodi nyingi na hivyo kupunguza sehemu kubwa
ya mapato anayopata mkulima.
(xi)
Kutokuwepo mpango maalum wa kupanua kilimo cha kahawa katika
maeneo ambako uzalishaji wa zao hilo unawezekana.
Kwa mfano, kuna maeneo katika mkoa wa Kagera, Mbeya, Ruvuma, Mara na
Kigoma ambako upanuzi huo unawezekana, lakini hatua za kupanua maeneo hayo
zinatekelezwa kwa kasi ndogo.
4. Ndugu
Mwenyekiti, haya ni baadhi tu ya matatizo yanayolikabili zao la kahawa. Ninafurahi kuona kuwa baadhi ya matatizo
yameanza kushughulikiwa kikamilifu na Vituo vya Utafiti wa Kilimo na Taasisi ya
Utafiti wa Kahawa (TACRI). Kwa mfano,
nina taarifa kuwa, uzalishaji wa kahawa ya vikonyo yenye ukinzani dhidi ya
ugonjwa Mnyauko Fuzari imeanza kuzalishwa kwa wingi ili kukabiliana na tatizo
hilo. Aidha, nimefahamishwa kuwa TACRI
imeainisha aina 31 za mbegu chotara za kahawa ambazo zina sifa ya kustahimili
mashambulizi ya ugonjwa wa chulebuni na kutu ya majani. Ninafikiri kuna haja ya kuongeza juhudi za
kupambana na magonjwa hayo ili magonjwa hayo yasienee nchi nzima.
5. Ndugu
Mwenyekiti, kuna baadhi ya wazalishaji ambao wanazalisha kahawa yenye ubora wa juu
na hivyo kupata abei nzuri.
Nimefahamishwa kuwa katika msimu wa 2002/2003, kahawa yenye ubora wa juu
ilifikia dola za Kimarekani 2.63 kwa kilo.
Hii inaonyesha kuwa, tukizalisha kahawa yenye ubora wa juu itapata bei
nzuri na wakulima watanufaika. Ni
dhahiri kuwa jambo hilo linawezekana.
Nitapenda Bodi iandae mkakati wa uzalishaji wa kahawa Bora. Kuna haja ya kuhakikisha yafuatayo
yanatekelezwa;
-
Kutoa elimu ya kuwawezesha Maafisa ugani kumudu kazi yao
vizuri zaidi.
-
Kuweka utaratibu mzuri zaidi wa kusimamia maafisa ugani.
-
Kusajili wakulima wote wa kahawa, ili kuhakikisha wanafuata
kanuni za kilimo bora cha kahawa.
Kuwasajili wakulima wa kahawa kutarahisisha kuwafikishia utaalam,
kusikiliza matatizo yao na kutafuta huduma za ufumbuzi wa matatizo
yanayowakabili.
-
Kuhimiza wakulima wa kahawa kujiunga katika vikundi ambavyo
vitasajiliwa kuzalisha kahawa ya ubora maalum (specialty coffee).
-
Kuweka mfumo wa wakulima kupata utaalam kutoka kwa wataalam
wa kilimo kwa mfano, kwa kutumia Mbinu Shirikishi Jamii na Shamba Darasa,
nakadhalika.
6. Ndugu
Mwenyekiti, sambamba na mpango wa kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa, Bodi
inatakiwa kuandaa mkakati wa kutambua na kupenyeza masoko ya kahawa ambayo
yatakuwa na soko zuri kwa kahawa tunayozalisha.
Inawezekana kuna masoko katika nchi za Afrika ambazo zinaweza kuwa soko
zuri la kahawa tunayozalisha na yasiyokuwa na vikwazo vingi. Lakini kwa kuwa hatujafanya juhudi ya kutosha
kuyatambua na kuandaa mkakati wa kupenyeza katika masoko hayo, tunabakia kutegemea
masoko ya ulaya Amerika na Japan ambayo yana vikwazo vingi.
7. Ndugu
Mwenyekiti, nimefahamishwa kuwa Taasisi ya Utafiti wa kahawa imekwisha kuandaa
Mpango wa Kuendeleza zao la kahawa.
Itakuwa vizuri kama mpango huo utahusisha wakulima wa kahawa na kufanya
utafiti utakaoleta mapinduzi katika uzalishaji wa kahawa nchini. Kwa muda mrefu uzalishaji wa kahawa umekuwa
wastani wa karibu tani 50,000 kwa mwaka.
Kuna haja ya kuongeza uzalishaji mara mbili ya uzalishaji wa sasa.
8. Ndugu
Mwenyekiti, soko la ndani la kahawa yetu bado ni dogo sana. Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa, tunakunywa
asilimia moja tu ya kahawa inayozalishwa hapa nchini. Nchi kama Ethiopia wanakunywa zaidi ya
asilimia hamsini ya kahawa wanayozalisha.
Kuna haja ya kuanza kuhamasisha wananchi kunywa kahawa na hususan kahawa
ya Tanzania. Itakuwa busara kama bodi
itaandaa mpango maalum wa kuhamasisha wananchi kujenga tabia ya kunywa kahawa.
9. Ndugu
Mwenyekiti, tarehe 2 Julai, 2003, nilipokutana na viongozi mbalimbali wa Wizara na
Taasisi zilizo chini ya Wizara ziliagiza kila Taasisi kuangalia upya muundo
wake na kuona kama unaiwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Kama Bodi ya Kahawa ilikuwa haijaanza
kutekeleza agizo hilo, ningependa kazi ya kwanza ya Bodi hii mpya ya Wakurugenzi
iwe kuangalia majukumu ya Bodi na Muundo wake na kuona kama muundo huo
unaiwezesha kutekeleza na kupata matokeo yanayokidhi matarajio ya
Serikali. Kuna haja ya kuangalia upya
ikama ya kila idara na kuhakikisha wote walioajiriwa ni wale tu wenye sifa
zinazotakiwa kwa mujibu wa majukumu ya Bodi.
Nitapenda baada ya zoezi hili kukamilika, Bodi kwa kushirikiana na
Halmashauri za Wilaya itafute utaratibu wa kuwatumia wataalam wa kilimo walio
chini ya Halmashauri badala ya kuajiri watumishi wapya.
10. Mwisho, baada ya kusema hayo,
ninatangaza kuwa Bodi ya Kahawa imezinduliwa rasmi.