HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA BENJAMIN WILLIAM MKAPA,
YA KUFUNGUA MKUTANO WA TATU WA WASHIKA DAU WA ZAO LA KOROSHO, SHIRIKA LA ELIMU
KIBAHA, PWANI, 29 SEPTEMBA 2001.
Mhe. Nicodemus Banduka, Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Waheshimiwa Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wabunge
Mheshimiwa Kitwana Kondo, Mwenyekiti wa Bodi ya
Korosho Tanzania,
Mabibi na Mabwana.
Nachukua
nafasi hii kuwakaribisheni nyote katika mkutano huu. Kwa kuwa mkutano ni wa siku
moja na unajumuisha Washikadau wengi ni vyema tukajiwekea nafasi ya kutosha
kusikiliza na kujadili kwa kina mada, zilizoandaliwa.
Mkutano
huu wa leo ni muhimu sana siyo tu kwa Washikadau mliojumuika hapa, bali ni kwa
wananchi wote wa Tanzania. Hii
inatokana na ukweli kwamba katika miaka ya karibuni zao la korosho limechangia
kipato kwa maelfu ya wananchi hususani wa Mikoa ya Kusini na Pwani na pia
kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni.
Katika
mazao ya biashara zao la Korosho linachuana na zao la kahawa ambalo liliongoza
kwa muda mrefu katika kulipatia taifa mapato.
Katika mwaka wa 1997/98 zao la kahawa liliingiza kiasi cha dola za
Kimarekani 108.7 milioni na korosho iliingiza dola 80.94 milioni, Mwaka wa
1999/2000 zao la korosho limeongoza usukani kwa kuliingizia Taifa fedha za
kigeni dola 123.8 milioni ukilinganisha na dola 73.6 milioni tu kwa zao la
kahawa. Bei ya kahawa kwenye soko
la dunia imeshuka sana, na ni vyema tukajizatiti kuongeza uzalishaji wa korosho
ambapo kwa sasa soko lake ni nzuri.
Pamoja na
mafanikio ambayo yamejionyesha katika zao la korosho miaka ya karibuni, kuna
matatizo ambayo yameendelea kutishia maendeleo ya sekta ya korosho. Matatizo
haya ni pamoja na kutokuwepo na uhakika wa soko, bei isiyotabirika, mfumo mbovu
wa upatikanaji pembejeo na uwezo mdogo wa ubanguaji nchini.
Hivyo basi kuyumba katika ufanisi wa sekta ya korosho kutaleta madhara
makubwa katika vita yetu ya kuondoa umasikini nchini na pia kuathiri uchumi wa
nchi yetu.
Aidha licha ya
kwamba tuna viwanda 12 vyenye uwezo wa kubangua tani 113,000 viwanda hivi
havifanyi kazi. Vile vile wawekezaji wa sekta binafsi katika kubangua korosho
bado ni wachache. Hadi sasa tunao
wawili tu ambao viwanda vyao vina uwezo wa kubangua tani 9,500 tu.
Kwa kuwa zao la korosho linaongoza katika kuliingizia nchi yetu fedha za
kigeni ni dhahiri kwamba iwapo matatizo haya hayatapatiwa ufumbuzi mapema
yatasababisha ufanisi katika sekta ya korosho kuyumba na kuathiri uchumi wa nchi
yetu na jitihada zetu za kuondoa umaskini.
Ni
mategemeo yangu kuwa baada ya mkutano huu matatizo mengi
ambayo yamekuwa yanakwamisha maendeleo ya zao la Korosho hususan katika
msimu unaokwisha yatapatiwa ufumbuzi kwani mengi ya majibu ya matatizo hayo yako
ndani ya uwezo wenu nyinyi kama Washikadau.
Hata
hivyo mikutano na warsha nyingi kuhusu kilimo zimefanyika nchini bila kuleta
mafanikio ya kutosha. Napenda kuona
mkutano huu uwe tofauti. Hivyo basi
ningependa baada ya kusikiliza mada zitakazotolewa majadiliano yatakayofuata
yalenge katika maeneo yafuatayo ambayo ni ya msingi na lazima yawekewe mikakati
thabiti ya kuendeleza sekta ndogo ya korosho.
Kwanza,
kuna umuhimu kwa washika dau wote tuliopo hapa kufanya tathmini ya kina kuhusu
matatizo ya zao la korosho nchini na kupendekeza hatua za msingi za kuchukuliwa.
Hatua hizo ziainishwe na kujulikana zichukuliwe na nani, na kwa muda gani.
Katika mchanganuo wa nani anapaswa kufanya nini, itabidi majukumu
ya vyombo mbalimbali vinavyoshughulikia zao la korosho yawekwe bayana, kwa lengo
la kila chombo kuelewa mipaka yake. Vyombo
hivyo ni pamoja na Bodi ya Korosho, Bodi yake ya Wakurugenzi, Mfuko wa
Uendelezaji Zao la Korosho (CIDEF), Vyama vya Ushirika, Umoja wa Wafanyabiashara
wa Korosho –“Cashewnut Association of Tanzania CAT”, Wauzaji
Korosho Nje (Exporters), Watafiti na pia Halmashauri za wilaya/Miji
zinazolima korosho. Majukumu na wajibu wa Serikali Kuu nayo ni vyema
yakaeleweka wazi kwa washikadau wote.
Pili,
takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa kiwango cha juu cha korosho kilichowahi
kuzalishwa nchini ni tani 145,000 katika msimu wa mwaka 1973/74.
Uzalishaji huu ulishuka kwa kasi kubwa hadi kufikia tani 16,500 katika
msimu wa 1986/87. Juhudi na hatua
mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kwa lengo la kufufua uzalishaji wa zalo
hili katika miaka ya tisini, zimezaa matunda mazuri ambapo uzalishaji wa korosho
umepanda mwaka hadi mwaka na kufikia kiwango cha tani 135,000 msimu wa
2000/2001. Kama tutajizatiti
kikamilifu upo uwezekano wa uzalishaji wa korosho nchini kufikia tani 400,000
ifikapo mwaka wa 2008. Kwa hiyo
pamoja na dalili hizi nzuri za kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hili hadi msimu
uliopita, bado kuna sababu za msingi mkutano huu kuangalia na kujadili hatua za
kuchukua ili uzalishaji uendelee kuongezeka na wakulima wetu wanufaike zaidi.
Hii ni pamoja na kuweka mifumo endelevu ya kutathmini mahitaji ya
pembejeo kwa kila msimu na mitandao ya uhakika ya uagizaji na usambazaji wake.
Hali iliyojitokeza msimu huu ya kuyumba bei na korosho kubakia mikononi
mwa wakulima kwa muda mrefu bila kuuzwa ni tishio kubwa kwa ukuaji wa zao hili,
na ni vizuri tukaijadili pamoja kwa makini na kujiwekea malengo ya muda mfupi na
mrefu ya jinsi ya kukabiliana na hali ya namna hiyo inapotokea, pamoja na
kuondoa vikwazo vinginevyo vya uzaliashaji
Tatu,
ikumbukwe kwamba nchi zinazozalisha korosho kwa wingi, mfano, India, Brazil na
Vietnam hubangua korosho zenyewe kabla ya kuuza nje.
Kwa hiyo ni lazima mkutano huu ujadili na kutoa ufumbuzi ili wakulima
wetu na taifa letu liweze kufaidika kwa:
·
Kuuza nje
korosho zilizobanguliwa ambazo soko lake ni kubwa zaidi na bei inayopatikana ni
nzuri kulinganisha na korosho ghafi.
·
Ongezeko
zaidi la thamani ya korosho, na kuwapatia ajira vijana wetu, hivyo kuongeza
vipato na kuchangia katika jitihada zetu za kupambana na umaskini.
·
Kutuwezesha
pia kupata bidhaa nyingine zitokanazo na korosho.
Katika jambo hili ni vizuri
tukawa na mikakati ya muda mfupi na mrefu ambayo itatuhakikishia kuwa siku za
usoni korosho zote zinazozalishwa nchini zitakuwa zinauzwa nje zikiwa
zimebanguliwa. Ubanguaji
ulenge kutumia viwanda vikubwa, vya
kati na vidogo.
Nne,
kuongezeka kwa uzalishaji wa korosho ni lazima kuende sambamba na kupatikana kwa
soko la uhakika kwa zao hili. Soko la zao hili ni pamoja na kuhamasisha soko la
ndani kwa matumizi ya zao hili pamoja na bidhaa zake. Kwa mfano, iwapo nusu ya
idadi ya Watanzania wote watakula angalau kilo moja tuu ya korosho
iliyobanguliwa kwa mwaka, karibu nusu ya korosho ghafi inayozalishwa nchini
itakuwa imetumika humu humu nchini. Aidha,
korosho zitumike kwa wingi zaidi katika mahoteli ya kitalii, tafrija na sehemu
mbalimbali za vinywaji. Inabidi
pawe na juhudi za makusudi za kuhamasisha upanuzi wa soko la ndani la zao hili.
Aidha ni muhimu tuainishe masoko mengine ya nje badala ya kutegemea
masoko machache kwa korosho ghafi tunazouza sasa. Ni mategemeo yangu kuwa
mkutano huu utajadili suala la soko la korosho zetu kwa mapana na marefu yake
kwani matatizo ya soko yaliyojitokeza msimu wa 2000/2001 yametufungua macho na
kutuonyesha ukubwa wa matatizo ambayo yako mbele yetu.
Tano,
kwa vile wote tunaelewa kuwa upo uwezekano wa kutumia bidhaa nyingine
zinazotokana na zao la korosho kuliko tunavyofanya hivi sasa, itakuwa ni jukumu
la mkutano huu kutoa na kujadili mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa mara moja
ili bidhaa hizo ziweze kutumika kwa ajili ya soko la ndani na la nje. Lazima watafiti wetu wachunguze zaidi matumizi mbalimbali ya
zao hili.
Sita,
kwa zao lolote kuwa na mafanikio ni lazima kuwepo na utafiti wa kina ambao
utasaidia kupata mbegu bora, miche bora na mbinu mbalimbali za kupambana na
magonjwa na wadudu. Kwa hiyo ni muhimu kwa Mkutano wetu kutafuta njia endelevu
za kupanua, kueneza na kugharamia utafiti wa kilimo cha korosho na bidhaa
zinazoweza kutengenezwa kutokana na korosho, pamoja na shughuli za ugani katika
zao hili.
Saba,
katika jitihada za kuhamasisha uzalishaji, ubanguaji na biashara ya zao la
korosho kwa ujumla ni muhimu kwa mkutano huu kutoa mapendekezo ya aina ya
vivutio na mazingira yatakayowavutia wakulima na wawekezaji wa ndani na nje
katika kilimo na ubanguaji wa korosho. Hata hivyo ni vyema pia mkapendekeza
jinsi ambavyo wawekezaji hao wataweza kusimamiwa ili watimize masharti ya
mikataba na taratibu zilizowekwa.
Mwisho,
ingawa yapo mambo mengi ambayo yanatakiwa kuzungumzwa kuhusu zao la korosho,
lakini ningependa haya niliyoyataja tuyazungumze na kuhakikisha tunayatolea
majibu na tunapotoka hapa kila mmoja wetu awe ameelewa njia iliyo sahihi ya
kuyashughulikia na wajibu wake.
Baada
ya kusema haya machache, sasa napenda kutamka kuwa mkutano wa tatu wa washika
dau wa zao la korosho umefunguliwa rasmi.
AHSANTENI
SANA