HOTUBA
YA WAZIRI WA KILIMO NA CHAKULA MHE. C.N. KEENJA (MB.) KWENYE MKUTANO WA TATU WA
WASHIKADAU WA ZAO LA MKONGE MJINI TANGA AGOSTI 25, 2001
-
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Benjamin W. Mkapa
ambaye ndiwe Mwenyekiti wa Mkutano huu
-
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Waziri
-
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa
-
Waheshimiwa Wabunge
-
Prof. A.S. Kauzeni Mwenyekiti wa Bodi ya Mkonge Tanzania
-
Ndugu S. Shamte Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Mkonge Tanzania
-
Washikadau wa zao la mkonge
-
Wageni Waalikwa
-
Mabibi na Mabwana
Mheshimiwa Rais wetu, awali ya yote ningependa kuchukua nafasi hii kwanza, kukushukuru sana, wewe binafsi Mheshimiwa Rais, kwa kukubali mwaliko wa washikadau wa zao la mkonge na kuja hapa Tanga kushiriki nao, katika mkutano wao huu wa mwaka. Karibu sana utufungulie mkutano huu. Aidha, tunashukuru sana pia kwa kukubali kubaki mkutanoni, ili kushiriki majadiliano kwa lengo la kufufua zao la mkonge. Akhsante sana. Pili, ningependa kuchukua nafasi hii pia kuwakaribisha wageni wote na washika dau walioalikwa kuhudhuria kikao hiki, ambao pia, tunatarajia watachangia mikakati madhubuti ya kufufua zao la mkonge, hivyo tunafurahi sana kuwa na wote hapa mkutanoni Tanga.
Mheshimiwa
Rais,
tunatiwa moyo sana kuona Kiongozi wetu Mkuu na Wasaidizi wako wa uongozi wa juu
wa taifa letu, kwa kujihusisha kwa karibu zaidi na sekta ya Kilimo na Mifugo.
Kwanza, wewe mwenyewe Mheshimiwa Rais, ulifungua mkutano wa washika dau,
wa zao la korosho kule Masasi mwezi Juni 2000.
Mnamo Desemba 2000, pia ulifungua mkutano na kuzindua Chama cha Kilimo na
Mifugo kule Arusha. Halafu, mwezi Machi tarehe 24 na 25, 2001 ulikuwa Mwenyekiti
wa mkutano wa washika dau wa sekta ya Kilimo, Dodoma. Tunapenda kukuhakikishia kwamba, mapendekezo yaliyotokana na
mikutano hiyo yameshaanza kufanyiwa kazi na Wizara ya Kilimo na Chakula, pia
taasisi zinazohusika. Pili, Makamu
wa Rais Marehemu Dr. Omari Ali Juma alikuwa Mwenyekiti kwenye mkutano wa sekta
ya Pamba mjini Mwanza. Tatu, Waziri
Mkuu, Mhe. Frederick T. Sumaye (Mb.) naye alifungua kikao cha sekta ya Kahawa,
mjini Moshi mwaka huu. Hii yote
inaonyesha jinsi gani uongozi wa juu, umedhamiria kuwahamasisha washika dau wote
katika kuendeleza kilimo ikiwa sekta kiongozi.
Sote wakulima tumefarijika sana.
Mheshimiwa
Rais,
Wizara ya Kilimo na Chakula, tayari imekwishatayarisha “Mkakati wa Kilimo”
yaani “Agricultural Sector Development Strategy” ambao utatumiwa
katika kutekeleza sera za kilimo. Hapa
ningewaomba washika dau wote wa zao la mkonge, kuisoma sera hii kwa makini, ili
Wizara ya Kilimo na Chakula ipate maoni yao.
Sambamba na sera hiyo, Wizara yangu pia imeshaziagiza Bodi zote za mazao
mbalimbali kutayarisha mipango yao ya miaka mitano toka mwaka huu hadi 2005.
Mipango hii inategemewa kuwasilishwa serikalini ifikapo mwezi Oktoba
mwaka huu lakini kabla yake inatakiwa ijadiliwe na washikadau pamoja na Bodi za
wakurugenzi husika.
Aidha, wakati Wizara yangu inaendelea kuboresha programu na mikakati madhubuti yenye kubaini aina ya vivutio na sera za kodi kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje wa zao la mkonge, ninapenda kutumia nafasi hii kuwakaribisha washika dau wote kutoa maoni yao, ili Bodi ya Mkonge iyajumuishe wakati inakamilisha mpango wake.
Mheshimiwa
Rais, Leo
tumekusanyika hapa kuzungumzia zao la mkonge.
Zao la wakati wa ukoloni lilikuwa maarufu kwa jina la “White Gold”
yaani “Dhahabu Nyeupe” umaarufu huo uliendelea mpaka kwenye miaka ya
1970. Wakati huo mkonge ulilimwa
katika mashamba ya hekta 475,000. Lakini
baada ya hapo zao hili limepungua sana ambapo leo tunazalisha jumla ya tani
20,000 tu yaani asilimia 2 tu katika mashamba yenye eneo la hekta 180,000.
Hiki ni kiasi kidogo mno ikilinganishwa na kiasi tulichoweza kuzalisha
mwaka 1964 ambapo zao lilifikia tani 230,000.
Kushuka huko kwa uzalishaji kumeathiri nchi kwa namna mbalimbali, maana
licha ya kupoteza ajira na mapato, mikoa ya Tanga na Morogoro ambayo ilikuwa
imeneemeka kwa ajili ya ukulima wa mkonge, imepunguza umaarufu wao mkubwa.
Leo hii nchini, bidhaa bandia, zimechukua zaidi ya asilimia 50 ya soko la
mkonge. Zao la mkonge pia limekuwa
likitegemea zaidi ya asilimia 75 soko la Ulaya Magharibi na Marekani ambapo
matumizi ya katani yamepungua sana.
Mheshimiwa
Rais,
Serikali ilipoanzisha sera mpya za uchumi mwaka 1985 kwa kiasi fulani
ilifanikiwa kufungua milango kwa kukaribisha wawekezaji kwa kuuza baadhi ya
mashamba yaliyokuwa yanamilikiwa na Mamlaka ya Mkonge (TSA).
Mpango huu. Ilipofikia mwaka 1998, zao la mkonge limekuwa linamilikiwa na
sekta binafsi kwa asilimia 100. Hata
hivyo, uzalishaji mkonge umekuwa ukipanda taratibu mno, maana hadi kufikia
mwishoni mwa mwaka 2000 uzalishaji umeongezeka hadi tani 20,489 ukilinganisha
kutoka tani 17,340 zilizozalishwa mwaka 1997.
Lakini Serikali inategemea kwamba wawekezaji wa ndani na nje, watatumia
kwa kikamilifu dhamana na vivutio, ambavyo serikali itakuwa inavitoa mara kwa
mara kwa kuendeleza Kilimo cha Mkonge. Katika
“Mkakati wa kuendeleza kilimo,” Kuinua ukuaji wa mazao ya biashara.
Kutoka asilimia 6.8 mwaka wa 2000 hadi asilimia 9 kwa mwaka,
ifikapo mwaka wa 2005, ni pamoja na uendelezaji wa zao hili la mkonge.
Mheshimiwa
Rais,
Hivi karibuni mimi mwenyewe na Naibu Waziri wangu, Prof. Mbawala (Mb.) tumepata
nafasi ya kutembelea baadhi ya mashamba na viwanda vinavyosokota kamba.
Tumejionea wenyewe juhudi za baadhi ya wawekezaji, pia mapungufu, ambayo
tutayafanyia kazi, kwa kuyarekebisha. Nimeridhika
na juhudi, ambazo zimeanza kufanywa katika upandaji na hasa kuwahusisha wakulima
wadogo wadogo kwenye zao la mkonge (outgrowers). Mheshimiwa Mwenyekiti,
wakulima wadogo wadogo wanaweza kulima mkonge kwa mpango huo, kwa hiyo
tunapendekeza wakulima hawa, wahusishwe kikamilifu na wawe na mkakati kamili wa
kuanzisha upanuaji wa kilimo hicho. Ili
kuongeza uzalishaji wizara itaendelea na harakati za kuendeleza kuhimiza
uanzishaji wa mitaji midogo (micro-finance) ya kugharamia shughuli za
kilimo ubia, kati ya wakulima wakubwa na wadogo, pia kuhamasisha Benki zetu
nchini, ziwe na Idara ya Mikopo kwa ajili ya Kilimo.
Lingine Mheshimiwa Rais, ni kwamba sekta hii ina uwezo mkubwa wa
kutengeneza bidhaa ambazo zinaweza kutumika humuhumu nchini, na hata nchi za nje.
Bidhaa kama kamba, mazulia na magunia yanaweza kabisa kushindana na
bidhaa zozote kutoka nje.
Hivyo
basi ni muhimu tukajadili ni jinsi gani tunaweza kuongeza juhudi zetu katika
kusindika malighafi ya mkonge na kuweza kuuza bidhaa zake badala ya singa za
mkonge peke yake, kama ilivyo leo hii, ambayo ni asilimia 2 tu ya matumizi ya
zao zima la mkonge. Kwa kuuza
bidhaa za aina nyingi zaidi mkonge utaweza kuchangia zaidi katika pato la Taifa
pia kupiga vita umaskini.
Mwisho
Mheshimiwa Rais,
naomba tena kutoa shukrani zangu kwako, kwa kukubali kuwa Mwenyekiti wa mkutano
wa leo na ninapenda kuchukua fursa hii, kwa heshima na taadhima, kukukaribisha
ili uweze kutufungulia kikao chetu hiki.