HOTUBA
YA KATIBU MKUU (BW. WILFRED NGIRWA) WA WIZARA YA KILIMO NA CHAKULA
Mhe.
Waziri wa Kilimo na Chakula, C.N. Keenja, (Mb),
Mhe.
Naibu Waziri, Prof. Pius Mbawala, (Mb),
Waheshimiwa
Wageni Waalikwa,
Wafanyakazi
wenzagu,
Mabibi
na
Mabwana.
1.
Napenda niwakaribishe wageni wetu wote
mliofika hapa kujumuika nasi katika sherehe yetu hii fupi ya uzinduzi
rasmi wa mbegu mpya zilizotafitiwa na wataalam wa Wizara hii.
Kama wengi wenu mnavyofahamu,
Wizara hii, kwa kupitia vituo vyake vya utafiti, imekuwa ikitoa aina mbalimbali
za mbegu bora kwa lengo la kuboresha kilimo cha wananchi wa Tanzania.
2.
Wote tunatambua umuhimu wa mbegu kama pembejeo yenye kipaumbele
katika kilimo. Hivyo basi
kwa mara ya kwanza Wizara sasa imeamua kuwa na sherehe maalum ya uzinduzi
wa mbegu mpya kila zitakapokuwa zimetolewa rasmi.
3.
Lengo kuu la sherehe yetu ya
leo ni kuwatangazia wakulima wa Tanzania kuhusu kuwepo
kwa mbegu mpya bora na pia kuwatambua na kuwaenzi watafiti waliofanikisha
upatikanaji mbegu hizo. Kwa kuwa
hii ni mara ya kwanza kuwa na shughuli ya aina hii vile vile tunawapongeza na
kuwatambua watafiti wote waliovumbua teknolojia bora hapo miaka ya nyuma.
4.
Mhe. Waziri nafurahi kutamka hapa kwamba mbegu utakazozizindua rasmi leo
zina sifa ambazo zitawezesha kuleta mapinduzi ya kilimo nchini na pia kuboresha
hali ya lishe, miongoni mwa wananchi wetu wengi hususani watoto.
5.
Mbegu mpya ya mahindi aina ya Uyole Hybird 615 (UH 615) inastahimili
ugonjwa hatari wa ukungu wa mahindi yaani "Grey Leaf Spot" ambao umekuwa tishio kwa kilimo cha mahindi
hasa Nyanda za Juu Kusini. Mbegu
hii yenye uwezo wa kutoa tani 8-10 kwa hekta itawezesha tena kilimo cha mahindi
chenye faida na tija.
6.
Mbegu mpya za mahindi za LISHE 1 na 2 zina virutubisho bora zaidi vya protein
ambavyo vitapunguza hali ya utapiamlo kwa watoto na pia kuweza kupunguza
gharama za utengenezaji vyakula vya mifugo.
Mbegu hii ina uwezo wa kutoa tani 8-10 kwa hekta.
7.
Mbegu ya mahindi aina ya SITUKA 1 na 2 zitaweza kuleta mageuzi makubwa
katika kilimo nchini. Mbegu hizi, siyo tu zinavumilia ukame kwa kiasi kikubwa sana,
bali pia zinastawi kwenye udongo wenye rutuba ndogo na kuweza kutoa mavuno ya
tani 3 hadi 4 kwa hekta. Hii ni
habari njema sana kwa wakulima wetu.
8.
Aidha mbegu mpya za mpunga za TXD 85 na TXD 88, zina sifa ya kuwa na
ladha nzuri na pia kutoa mavuno mengi ya tani 6-8 kwa hekta.
9.
Mheshimiwa Waziri na Wageni waalikwa kazi kubwa iliyo mbele yetu ni
kuhakikisha mbegu hizi zinazalishwa kwa wingi ili ziweze kuwafikia wakulima
katika muda mfupi ujao.
10.
Sote tunafahamu kuwa
shughuli za utafiti wa kilimo huchukua muda mrefu na hugharimu fedha nyingi.
Kwa kuwa utafiti ni mojawapo ya majukumu muhimu sana ya Wizara, basi
tutahakikisha tunatenga fedha za kutosha kuendesha utafiti na vile vile
tutashirikisha kikamilifu wadau wote na wahisani katika suala hili.
11.
Mkakati wa
kuendeleza kilimo nchini (ASDS) unaainisha maeneo yatakayopewa kipaumbele katika
utafiti na jinsi wadau mbalimbali
watakavyohusishwa katika uchangiaji wa gharama za utafiti.
Miradi na programu mbalimbali zinazoandaliwa kati ya Wizara na Wahisani
zinaweka mkazo kwenye kuboresha huduma zetu ikiwemo utafiti.
12.
Kwa kumalizia
ningependa nitoe pongezi zangu binafsi na pia kwa niaba ya uongozi wa Wizara kwa
wataalam wetu kwa kazi zao nzuri za kubuni teknolojia bora za kuendeleza kilimo
nchini. Tunatambua jinsi kazi hizo
zinavyofanyika katika mazingira magumu. Nawaomba
waendeleze moyo huo wa uzalendo wakati Wizara inaendelea
na jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira yao ya kazi pamoja na
maslahi yao.
13.
Zawadi wanazopewa baadhi yao leo ni kielelezo cha Wizara kutambua
na kuenzi jitihada hizo. Aidha
ieleweke kuwa zawadi hizo watakaozipokea ni kwa niaba ya wote waliohusika.
Wizara vile vile inatambua michango ya Idara na Taasisi zake.
14.
Ningependa pia niwashukuru wote wale wanaoshirikiana na Wizara hii kwa
hali na mali kuendeleza kilimo chetu. Napenda
kutambua michango ya mashirika, Taasisi na nchi zifuatazo:- FAO, Benki ya Dunia,
JICA, NORAD, DANIDA, DFID, Netherlands, USAID, GTZ, Ireland AID, EU, SACCAR,
ASARECA, CIAT, CIMMYT, ICRISAT, ICRAF na IRRI.
15.
Nategemea kuwa kufanyika kwa sherehe hii leo pamoja na utoaji wa vyeti na
zawadi itakuwa ni changamoto kubwa kwa watafiti wote nchini kuongeza bidii
katika kazi zao. Sambamba na hili nategemea wakulima wetu watazitumia mbegu
hizi mpya ili wanufaike na zile sifa nzuri nilizozitaja hapo awali.
Nawashukuru kwa kunisikiliza.