HOTUBA
YA UZINDUZI WA MRADI “DAI PESA”
KWA MKOA WA
MHE. PIUS P. MBAWALA (MB) NAIBU WAZIRI KILIMO
NA CHAKULA ILIYOFANYIKA UKUMBI WA DON BOSCO MJINI SONGEA
TAREHE
11 MACHI, 2004
-
Ndugu Mwenyekiti Maj. Gen. S.S. Kalembo,
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma;
-
Bwana Joe Burke Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa DAI
PESA;
-
Ndugu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma;
-
Ndugu Wakuu wa Wilaya Mbinga, Songea na
Namtumbo;
-
Wakurugenzi wa Wilaya Songea, na Mbinga;
-
Wakuu wa Idara za Serikali na Halmashauri;
-
Wawakilishi wa Mashirika na Miradi mbalimbali
Mkoani Ruvuma;
-
Wawakilishi wa sekta binafsi;
-
Wawakilishi wa vikundi vya wakulima;
-
Wanaushirika;
-
Wasimamizi wa Mradi wa DAI PESA;
-
Mabibi na Mabwana.
Kwanza
napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru sana viongozi wa “DAI PESA” kwa kuwaalika
mhudhurie hafla hii ya uzinduzi wa mradi huu.
Aidha, nawashukuru viongozi wa “DAI PESA” kwa kunipa mimi heshima ya
uzinduzi wa mradi huu mkoani Ruvuma siku ya leo. Aksante sana kwa kunialika.
Mimi
binafsi ninaufahamu sana mradi huu wa “DAI PESA” kwa sababu mimi ndiye
niliyeuzindua rasmi kitaifa kule Dar es Salaam, mwaka jana tarehe 27 Februari,
2003. Siku hiyo nilishirikiana na Balozi
wa Marekani wa wakati ule Bwana Robert Royall.
Ila nasikitika tu kwamba mradi huu umecheleweshwa kuanza shughuli hapa
kwetu mkoani Ruvuma. Hata hivyo ingawa
umechelewa kutufikia lakini leo hii mradi unaingia mkoani mwetu tujipongeze kwa
hilo na nimshukuru sana Bwana Joe Burke, Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa “DAI PESA”
kwa kutujumuisha nasi Ruvuma katika mradi huu muhimu kwa sekta ya kilimo.
Awali ya yote napenda kwanza
nifafanue nini maana ya “DAI PESA”? Neno “DAI” kirefu chake kwa kiingereza ni
“Development Alternatives Incorporated” ikiwa na tafsiri ya “Asasi ya
Maendeleo” ambayo ndiyo inasimamia mradi wa “PESA”. Kirefu cha neno “PESA” kwa
kiingereza ni “Private Enterprise Support Activities” tafsiri yake ni
“Usaidiaji wa uendeshaji wa shughuli za biashara binafsi”. Uzinduzi wa “DAI PESA” Ruvuma unafanyika leo
hapa Don Bosco na sisi sote tuliokusanyika hapa ni mashahidi wa tukio hilo.
Mradi
wenyewe unahisaniwa na Shirika la Maendeleo la Marekani yaani USAID.
Utekelezwaji wa mradi DAI PESA umefanyika katika mikoa sita ikijumuisha mikoa
ya Tanga, Morogoro, Iringa, Rukwa, Mbeya na kuanzia leo mkoani kwetu Ruvuma. Mradi umeanza mwaka 2003 na utakoma mwaka
2006. DAI PESA ni mradi wenye baraka za
Serikali yetu kupitia Wizara ya Fedha ambayo iliyotia sahihi kwa niaba ya
Serikali, na DAI PESA inahusisha Wizara nyingine tano.
Lengo
la mradi wa DAI PESA ni kuunga mkono juhudi za shughuli za sekta binafsi nchini
lakini lengo la Mradi SIYO KUTOA PESA kwa washiriki shughuli za mradi huu. Kwa maneno mengine DAI PESA ni mradi wa
kuwahamasisha na kuwapa maarifa washiriki mradi jinsi ya kuboresha shughuli
halali za kilimo kibiashara kwa kutumia mbinu za kisasa.
Hivyo madhumuni ya uzinduzi wa mradi huu na WARSHA hii ni kutuelezea sisi
wadau/washiriki kuhusu DAI PESA:-
1.
Jinsi mradi utakavyotekelezwa.
2.
Kujua mahitaji ya walengwa wa mradi wa DAI PESA hasa
kuhusiana na mafunzo ya uwezo wa kuimudu biashara (Training needs
assessment). Vipengele vya mradi huu
vitafafanuliwa na wataalam wa mradi katika warsha hii leo.
Hapa kwetu mkoani Ruvuma, DAI PESA itajihusisha na sekta binafsi kwenye
sekta ya kilimo hususan wakulima wadogo wadogo na wale kutoka sekta ya Mali
Asili yaani shughuli za uvuvi. Hivyo
katika mkoa wa Ruvuma mradi wa DAI PESA utaunga mkono sekta ya kilimo kwa
kuanzia na uendelezaji bora wa biashara ya Pilipili kichaa, Korosho, Paprika,
pamoja na uvuvi na uuzaji wa samaki kutoka ziwa Nyasa. Mafanikio ya mradi wa DAI PESA unategemea
sana ushirikiano wa wadau wote wakiwemo viongozi wa Serikali Kuu, Halmashauri
za wilaya, pamoja na sekta zilizochaguliwa.
Ndugu Mwenyekiti, kama nilivyokwisha kueleza hafla hii ya leo ina lengo
la kuzindua Mradi wa DAI PESA ambao utaelekeza nguvu zote katika kuendeleza
shughuli za kilimo ambao sisi sote tuliomo hapa ni wadau wakubwa. Kwa Tanzania kilimo ni ndicho uti wa mgongo
wa uchumi wetu. Katika serikali ya awamu
ya tatu pamekuwepo na mageuzi makubwa sana ya shughuli za uchumi katika sekta
nyingi ikijumuisha ile ya kilimo, utalii, madini, viwanda na biashara shughuli
sekta ambazo zimeongeza sana mapato kwa taifa pia zimetoa ajira kwa watu
wengi. Aidha mageuzi hayo makubwa ya
uchumi yameteremsha sana mfumuko wa bei asilimia 30 hadi kufikia asilimia 4 tu.
Aidha Serikali
yetu inahimiza sana kuendeleza uzalishaji katika kilimo kama mkakati wa kukuza
uchumi miongoni mwa wakulima, pia katika sekta binafsi kwa kuwa kukuza kilimo
ni kunawanufaisha wananchi ambao kwa asilimia 85 huishi vijijini. Kilimo pia huchangia asilimia 50 ya pato la
Taifa (GDP). Vile vile, kilimo ni chanzo
kikuu cha ajira nchini kwa asilimia 80 kutokana na shughuli za uzalishaji na
usindikaji wa mazao ya kilimo, shughuli ambazo kwa kiasi kikubwa hutupatia
fedha za kigeni pia kutulisha. Nchini
kilimo sasa kinatoa mazingira mazuri kwa wawekezaji ambao shughuli zao husaidia
sana kukuza uchumi wetu, hasa katika mkakati wa kuondoa umaskini (PRSP)
na kuboresha maisha ya wananchi wetu kulingana na Dira ya Maendeleo (Tanzania
Development vision 2025). Dira hiyo
imeweka wazi lengo la ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 8 kwa mwaka.
DAI PESA ina
nafasi yake katika kuunga mkono shughuli za uzalishaji unaolenga upatikanaji
masoko ambayo yatakuza biashara ya mazao katika sekta ya kilimo na hivyo
kuboresha maisha ya wananchi vijijini.
Ikizingatia kuwa wananchi vijijini hawana ujuzi wa kisasa katika mbinu
bora za kilimo wala utaalam wa kisasa wa biashara. Wakulima pia wanahitaji aina
mbalimbali za mbegu bora, upatikanaji wa pembejeo, mikopo na masoko. Aidha
kilimo kinahitaji ujuzi katika uwekezaji, uzalishaji, usindikaji na hatimaye
uongezaji thamani wa mazao, hasa tukikumbuka kuwa uuzaji nje wa mazao yetu
yasiyosindikwa kunaudhuru uchumi wa Tanzania.
Kwa kushirikiana na DAI PESA,
serikali, vile vile sekta binafsi, pamoja na wahisani tutaleta
mabadiliko makubwa ya uchumi vijijini. DAI ina mkakati wa kuleta mabadiliko
hayo kwa kuwapa wakulima mafunzo katika mbinu za kisasa na kwa kuwahamasisha
wakulima kupitia kujiunga katika vikundi na hivyo wanufaike na faida ya umoja
katika upatikanaji wa bei nzuri kwa mazao yao watakayozalisha.
DAI, kwa
kuwaunganisha wakulima na masoko inalenga pia kusaidia kuleta ushindani katika
masoko ili kuwapatia wakulima bei nzuri zaidi.
Taarifa za masoko ni muhimu kwa wakulima kwani huwawezesha kuchagua lini
na wapi, wauze kwa faida kubwa, Aidha huwasaidia wakulima kujua wapi mikopo na
mitaji inapatikana, na namna ya kujitafutia pembejeo kwa wakati ili iwanufaishe
wao wakulima badala ya wanunuzi wa mazao yao.
DAI pia itawaelimsha watumishi wa Serikali vijijini, katani,
tarafani, wilayani na mkoani na hivyo kusaidia katika kuimarisha ushirikiano
kati ya serikali na sekta binafsi. Washiriki wengine katika huduma za biashara
ndogo ndogo, na asasi za biashara kama CCIA nao wataimarishwa. Lengo ni kushirikisha wadau wote kusudi
pasiwepo na upotevu wa rasilimali.
Tegemeo la DAI ni kuwa ifikapo mwaka 2006 mradi uwe umewaandaa wakulima
kunufaika na malengo yaliyokusudiwa. Kwa
kufanya hivyo DAI itakuwa imetekeleza malengo ya USAID, DAI PESA na Ilani ya
uchaguzi ya CCM (2000) inayosema, “Kilimo cha kisasa ndio ufunguo wa maendeleo
ya uchumi wote wa nchi yetu. Kilimo cha
kisasa kitaongeza tija na kutoa ziada kubwa.
Kutokana na hali hiyo, CCM, katika kipindi cha miaka mitano ijayo
itaendeleza juhudi zake zilizoanza miaka ya nyuma za kukienzi na kukiendeleza
kilimo kwa kuhakikisha kuwa kanuni za kilimo zinafuatwa, zikiwemo zile za
matumizi ya zana za kisasa na pembejeo” ……(2000:11).
Hata hivyo
pamoja na malengo mazuri ya DAI PESA ningependa kuwashauri wahisani wa mradi
wetu kwamba ni vizuri wakazielewa kiusahihi sera zetu za biashara nchini na
mikakati mbalimbali ikijumuisha: Mkakati wa sekta ya kilimo au “Agricultural
Sector Development Strategy (ASDS)” na Mkakati wa programu ya sekta ya kilimo
au “Agricultural Sector Development Programme (ASDP)” na Sera ya kuondoa
umaskini nchini, mambo ambayo pia yangeweza kuwa chanzo cha mitaji ya uwekezaji
katika baadhi ya shughuli za DAI PESA.
Aidha,
utekelezaji wa Mradi wa DAI PESA ufanyike kupitia viongozi na watumishi
mbalimbali wa kilimo (yaani DALDO na wenzake) waliopo katika wilaya husika ili
kukwepa kuunda vyombo au taasisi mbadala.
DAI PESA iwatumie kikamilifu maafisa wetu wote wa ugani katika ngazi
zote za uongozi husika vijijini na wilayani. Pia DAI PESA isaidie kuimarisha
uwezo sio wa wataalam pekee yake bali
wawakilishi wote wa wakulima ikijumuisha madiwani na viongozi katika ngazi
za kijiji na mamlaka zilizoko katika Halmashauri husika na kwa kufanya hivyo
mradi wa DAI PESA utakapoisha hapo 2006 wakulima, maafisa Ugani na Mamlaka
mbalimbali husika vijijini hadi wilayani watakuwa tayari wamekwisha jengewa
uwezo wa kujiendeleza wenyewe.
Mwisho, naomba nisisitize tena
kuwa “DAI PESA” ni kifupi cha maneno ya kiingereza niliyokwisha yataja hapo
awali hivyo isimaanishe kuwa wakulima wetu “WATAKE AU WADAI PESA”
(Demand money) kutoka kwa mradi, au USAID au Mbunge au Serikali, bali DAI PESA
ni mradi wa utaratibu wa kuwapa wakulima maarifa na mbinu za biashara pia kupewa fursa ya masoko. Aidha,
ninashukuru sana DAI PESA kwa heshima niliyopewa ya kuzindua mradi huu. Tena
niwapongeze sana wote mnaoshiriki katika warsha hii, na hasa viongozi na
wahisani wa DAI PESA waliogharimia warsha hii ambayo naitakia mafanikio.
Mwenyekiti, baada ya kusema yote
haya, sasa napenda kutamka rasmi kuwa, warsha hii ya DAI PESA imezinduliwa
RASMI. Aksante sana kwa kunisikiliza.